MADEREVA WALILIA MAFUNZO,WATAKA WAFIKISHIWE VIJIJINI-KAGERA
Kibuka Prudence,Muleba(0756 872135)
BAADHI ya wamiliki wa vyombo vya moto wilayani Muleba mkoani Kagera,wameiomba serikali kuendeleza mafunzo ya muda fupi ya udereva ili kuepusha ajali zinazotokea mara kwa mara ambazo mara nyingi usababishwa na baadhi ya watumiaji wa vyombo hivyo kutojua sheria n a taratibu za uendeshaji.
Rai hiyo ilitolewa na wahitimu wa mafunzo ya awali ya udereva,katika risala iliyosomwa kwa niaba yao na bi.Prasidia Malinzi,ambapo zaidi ya wahitimu 100 kutoka kata za Kyebitembe,Karambi na Nshamba wilayani Muleba walihitimu mafunzo hayo na kutunukiwa vyeti na kaimu Kamanda wa jeshi la Polisi Vitus Mlolere,mwishoni mwa juma.
Madereva hao waliupongeza utaratibu wa kupeleka mafunzo vijijini, uliofanywa na jeshi la Polisi mkoani hapa kupitia kikosi cha usalama barabarani kwa kushirikiana na chuo cha mafunzo ya udereva cha Lake Zone Driving School cha mjini Bukoba.
Walisema kuwa kwa kipindi hiki ambapo jamii imekuwa na kasi katika manunuzi ya vyombo vya moto ambavyo ni pikipiki na magari,hakuna budi utaratibu huo ukaendelea ili kuelimisha watumiaji wa vyombo hivyo kwani wengi wanavitumia bila kujua sheria za udereva na usalama wao pia.
"Tunaomba elimu hii iendelee katika jamii yetu ili kuepusha ajali za mara kwa mara,tunaamini kwa kufanya hivi tutaepusha vifo vingi vinavyotokana na ajali"alisema Albogast Rushekya mmoja wa wahitimu wa mafunzo hayo.
Kwa upande wake mkurugenzi wa chuo cha udereva cha Lake Zone Driving School Winstone Kabantega,alisema mafunzo hayo yameendeshwa katika vituo viwili ndani ya wilaya ya Muleba ambavyo ni kata ya Kyebitembe na kata ya Nshamba,ambapo wahitimu wamejifunza kwa muda wa siku tano,na tayari yamekuwa yakiendeshwa katika sehemu mbalimbali kulingana na wahitaji mara baada ya kuomba huduma hiyo.
Kabantega alisema kuwa mafunzo hayo yanaendeshwa kwa ushirikiano baina ya jeshi la Polisi mkoani Kagera na chuo cha Lake Zone Driving School,ambapo chuo kinatoa wakufunzi na jeshi la Polisi linatoa wataalamu kupia kikosi cha usalama barabarani.
Alisema kuwa moja ya malengo makuu ya mafunzo haya ni kuwafikishia wamiliki wa vyombo hivi mafunzo ya udereva popote pale wanapoona wanaweza kujipatia mafunzo ili kupunguza gharama ya kuyafuata katika vyuo ambavyo vinakuwa mbali na maeneo wanamoishi.
Aidha,Kabantega alisema kuwa mafunzo haya ni mwendelezo hasa baada ya kuwepo mabadiriko ya reseni ambavyo madereva wengi walikuwa nyuma kukidhi mahitaji ya kufuata utaratibu wa kujipatia reseni mpya.
No comments:
Post a Comment