Thursday, March 22, 2012

WIKI YA MAJI BILA MAJI............

Kwa miaka mingi serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha wananchi tunapata maji safi na salama. Maadhimisho ya wiki ya maji ni mojawapo ya jitihada, ambapo kwangu mimi naona inalenga kutoa elimu na fursa kwa wadau mbalimbali weweze kujadili namna ya kuboresha huduma hii hasa kwa maeneo ya vijijini ambapo imendeelea kuwa ndoto. Swali ni kuwa, kwetu sisi wananchi maadhimisho ya maji yanapaswa kutusaidia nini?
Nauliza swali hili kwa kuwa tumeshuhudia mengi yakifanywa kwa lengo la kuboresha huduma ya maji lakini bado matokeo ya juhudi hizi hayajatufikia sisi wananchi.
Wiki iliyokwisha, Umoja wa Mataifa ulizindua ripoti ya kimataifa ya hali ya upatikanaji huduma ya maji. Ripoti hiyo inaonesha kuwa kimataifa malengo ya milenia kuhusu maji yamefikiwa, ambapo asilimia 89% ya watu duniani wanapata maji kupitia vituo vya maji (vichoteo vya maji) vilivyoboreshwa.
Wakati dunia ikifurahia hatua hii nzuri, hali ni tofauti hapa kwetu Tanzania. Ripoti inaonesha kuwa hali ya huduma ya maji imekuwa ikidhorota na hata kupungua badala ya kuwa bora. Ripoti hiyo inaonesha kuwa asilimia 53% (mwaka 2010) ya watu hapa Tanzania wanapata huduma ya maji kutoka vituo vilivyoboreshwa. Huduma hii imepungua kwa asilimia 2% ambapo mwaka 1990 watu asilimia 55% walikuwa wanapata huduma ya maji.
Kwa mlinganisho, ripoti inaonesha kuwa ni nchi kumi na moja tuu zenye hali mbaya ya upatikanaji maji duniani kuliko Tanzania. Picha hii inazidi kuwa mbaya tunapolinganisha hali yetu ya huduma ya maji na nchi tisa za Afrika Mashariki.
 Mwaka 1990, tulikuwa nyuma ya nchi mbili tu Burudi na Rwanda kwenye upatikanaji wa maji safi na salama. Lakini kwa ripoti hii ya mwaka 2010, Malawi, Uganda, Zambia na Kenya zimetupita kwenye utoaji wa huduma ya maji. Sasa ni Msumbiji na Ethiopia tu ndio zipo nyuma yetu kwa utoaji wa huduma za Maji.
Ikumbukwe kuwa, katika kipindi cha miaka 20, 1990 hadi 2010, serikali imechukua jitihada mbali mbali ili kuboresha huduma ya maji nchini. Jitihada hizo ni pamoja kuanzisha sera ya maji, ambapo sera hii ilifanyiwa marekebisho mwaka 2002 na kufanya maji kuwa bidhaa na sio huduma.
Sera hii ililenga kuwashirikisha wananchi katika kusimamia na kuendesha miradi ya maji. Pia serikali imekuwa ikiongeza bajeti ya maji mfano bajeti ya maendeleo ya maji vijijini iliongezeka kutoka 19bilioni mwaka 2005/06 hadi 124 bilioni mwaka 2009/2010.
 Sambamba na ongezeko la bajeti, Programu ya Mendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP). Program hii imekuwa na awamu mbili ambapo awamu ya kwanza kulikuwa na miradi ya matokeo ya haraka (Quick Win Projects) na awamu ya pili miradi ya vijiji kumi kila wilaya maarufu kama miradi ya benki ya dunia.

Jitihada hizi zimehusisha rasilimali nyingi sana za ndani na nyingine ni misaada na mikopo. Lakini bado matokeo ya jumla katika kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji Tanzania yamezidi kuwa hafuifu kama ambavyo ripoti hii inavyoonesha. Je, tunakosea wapi? tuendelee kuwekeza kwenye hii sekta isiyokuwa na matokea chanya?
Kwa hali hii gari linakuwa linarudi nyuma badala ya kwenda mbele. Wizara ya maji, na wadau wote wa maji tufanye nini kuboresha hali hii? Je tunafahamu kiini cha tatizo? Kwa mtazamo wangu mojawapo ya tatizo ni kutodumu kwa miradi ya maji.
Tumekuwa tukiwekeza kila mwaka kujenga miradi mipya ya maji, lakini juhudi zetu zimekuwa zikienda sambamba na kufa kwa miundombinu ya maji.
Sensa ya utambuzi wa vituo vya maji iliyofanywa na GEODATA na WaterAid mwaka 2005 hadi 2009 kwenye wilaya 48 inaonesha kuwa asilimia 44% ya vituo vya maji vilivyoboreshwa havifanyi kazi. Sensa hiyo pia inaonesha kuwa, kila baada ya miaka miwili asilimia 25 ya miradi ya maji inakuwa tayari imeshakufa. Je ni kwanini miradi ya maji haidumu?
Imefika wakati sasa tuache kuwekeza katika kujenga miradi mipya ya maji, badala yake tuongeze jitihada na rasilimali hizo katika kufufua miradi iliyokufa na kuweka mfumo wa kufanya miradi iwe endelevu. Kwa hali ilivyo sasa, shabaha kubwa ya serikali imekuwa kujenga miradi mipya ya maji kuliko kuidumisha na kufufua miradi iliyopo.
 Mfano mdogo ni Kijiji cha Kipaduka, kilichopo kata ya Uhambingeto wilaya ya Kilolo ambapo kijiji hiki ni mojawapo ya vijiji kumi vitakavyopata mradi wa benki ya dunia. Kipaduka wamehamasishwa na wameunda kamati ya maji na kuchangisha shilingi milioni sita ambazo zipo benki zaidi ya miaka miwili sasa. Lakini kijiji kina vituo 10, nane havifanyi kazi na kamati haioni kuwa wanawajibika kutengeneza hivi vituo vilivyoharibika kwa vile wao wameandaliwa kwa ajili ya kusimamia mradi mpya.
 Hii inaonesha jinsi gani tupo tayari kujenga miradi mipya kuliko kuendeleza tuliyonayo.
Changamoto nyingine ya kuzingatia ni aina ya teknolojia tunayotumia na vipuli vyake. Jamii zimekuwa zikilalamika kuwa mashine na vifaa mbalimbali vya maji vimekuwa vikifa mara kwa mara.
Hali hii sio tu kwenye sekta ya maji, bali tumekuwa tukishuhudia bidhaa nyingi feki zikiingizwa hapa nchini. Hii inapelekea kuongezeka kwa gharama za uendeshaji wa miundombinu ya maji na kuwafanya wanajamii kushindwa kumudu. Hivyo serikali inapaswa kuchukua hatua ili kudhibiti haya.
Zipo sababu nyingi zaidi zinazosababisha miradi ya maji kufa mara kwa mara kama uelewa mdogo wa wanajamii katika kuiendesha miradi ya maji, halmashauri kukosa fedha za ufuatiliaji, na mengineyo. Cha msingi wadau wote tuibebe changamoto hii na kuifanyia kazi. Maadhimisho ya wiki ya maji yawe chachu katika kuleta kujadili changamoto hizi. Tukumbuke wananchi hawahitaji mipango, sera, magari, au hadithi nyingine zozote…wanahitaji maji.
Makala haya yamechapichwa kwenye Gazeti la Kwanza Jamii-IRINGA
Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa baruapepe richardlucas@daraja

No comments:

Post a Comment